Wengi wamejikuta wakiitwa wahuni kutokana na kuwa na
uhusiano wa kimapenzi na makundi ya wanaume au wanawake. Hata hivyo
wachunguzi wa masuala ya mapenzi wanasema idadi kubwa ya wapenzi si
kigezo sahihi cha kupima tabia ya mtu na kumhusisha na uhuni.
Watalaam
hao wanataja safari ya kupata chaguo halisi la mwanaume/mwanamke wa
maisha ndiyo inayowaponza wengi kiasi cha kujikuta wameingia katika
kashfa ya kuwa na uhusiano na dazeni ya wapenzi.
Wanasema
msichana/mvulana anayeingia katika uwanja wa mapenzi kwa kuwa na hisia
za kufanya ngono, hukosa umakini wa nani anafaa kuwa mpenzi wake
kutokana na kukosa elimu ya uhusiano kutoka kwa wazazi wake.
Kwa
mantiki hiyo, bila upembuzi wa kina, mtu asiye na elimu ya jinsi ya
kumpata mpenzi wa kweli hujikuta ameangukia kwa mwanaume/mwanamke
asiyemfaa, ambapo baadaye huamua kuachana na huyo na kwenda kwa mwingine
kujaribu bahati tena ya kupata penzi la kweli.
Zinatajwa
zawadi, hitaji la kusaidiwa kimaisha, mvuto wa kimahaba na mazoea kuwa
ni vichocheo vinavyowaangusha wengi kwenye mapenzi na wasiowafaa.
Ukweli
ni kwamba mtu aliyenaswa kwa ‘ujinga’, huwa hakatwi kiu ya penzi na
mwanaume/mwanamke asiye chaguo sahihi la maisha yake. Hivyo hufikia
maamuzi ya kujiingiza katika uhusiano mpya mara 2,3,4,5 na kujikuta
wakiambulia wanaume/wanawake wale wale wasio sahihi kwake.
Mwanamnke
mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Suzzy aliwahi kuniomba ushauri,
akasema amechoka kuchezewa, maana kila mwanaume anayempata anakuwa si
chaguo lake. Lakini kibaya zaidi kuachia ngazi au kutemwa huku akiwa
tayari ameshafanya mapenzi na wanaume hao.
Nia ya swali
lake ilikuwa ni kuniomba njia za kumtambua mwanaume mkweli bila kufanya
naye mapenzi? Aliuliza hivyo huku akiwa na hoja kuwa wanaume wengi
hawako tayari kuwa na uhusiano na msichana bila kufanya naye mapenzi na
wakati huo huo huficha tabia zao chafu wakilenga kumnasa wamtakaye.
Binafsi
nafahamu kuwa kuna wanawake/wanawake wengi ambao hujiingiza katika
mapenzi kwa kutekwa na hadaa za mwili na kujikuta wanacheza mchezo wa
kitoto wa pata potea.
Ni madhumuni ya somo hili
kufundisha vigezo vya kumpata mwanaume/mwanamke halisi wa maisha, bila
kufanya naye mapenzi. Njia hii ina faida kwa pande zote mbili yaani kwa
mwanamke na mwanaume kwani kuacha au kuachwa bila kufanya mapenzi ni
bora kuliko kuwa muonjaji, tabia ambayo huathiri kisaikolojia na ni
hatari kwa afya.
Ifuatavyo ni njia ya kisaikolojia
ambayo mwanamke anaweza kutumia kumpata mwanaume mwenye kumfaa bila
kufanya naye mapenzi tena ni jibu sahihi la kuondokana na mchezo wa
kubahatisha kwa wanaume wanaosaka wapenzi wa kweli na si taksi bubu
ambazo mchana huweka namba za njano usiku nyeusi.
KWANZA- Ni
ya mwanamke/mwanaume mwenyewe kujifahamu na kufahamu vigezo vya mpenzi
anayemhitaji katika maisha yake. Ifahamike kuwa kila mwanaume ana wake
na kila mwanamke anaye wake wa maisha pia. Hivyo asiyekufaa wewe
anawafaa wengine, kinachotakiwa ni wewe kujitambua kwanza ili umtambue
umtakaye.
Wanawake/wanaume wengi hawafahamu wanahitaji
wapenzi wa aina gani, hivyo wanajikuta kama watu wanaoingia sokoni bila
kujua wanataka kununua nini? Ndiyo maana wengi wameangukia kwa matapeli
wa mapenzi, wakachezewe na kuumizwa moyo bure.
PILI- Ni
kuketi chini na kuorodhesha vigezo stahili vya mwanaume/mwanamke
unayemtaka. Baada ya hapo orodhesha tena kasoro za mwanaume/mwanamke
unazoweza kuzivumilia na zile ambazo huwezi kuzivumilia kabisa. Hii
inatokana na ukweli kwamba mwanadamu hajakamilika, ana upungufu wake.
TATU- Anza
kumsaka kwa kutumia milango ya fahamu. Cha kufanya hapa ni kuruhusu
macho yawaone wanaume/wanawake na kuwatathmini kwa maumbile yao ya nje
na kisha kupata majibu kutoka moyoni juu ya kuvutia kwao ambako
hutambulika kwa moyo kurithika na mwili kusisimka.
NNE - Kuanzisha
safari ya kuchunguza tabia za nje na za ndani kivitendo. Hapa suala la
ukaribu baina ya mwanaume na mwanamke linahitajika. Msingi unaotajwa
hapa ni kujenga mazoea ya kawaida yasiyokuwa na masuala ya kimapenzi na
ngono. Kutambuana, dini, viwango vya elimu, kabila na makundi ya
marafiki ni mambo ya kuzingatia.
Katika uchunguzi huu
mwanamke/mwanaume anayetafuta mpenzi hana budi kupitia na kumlinganisha
huyo aliyempata na vigezo alivyojiwekea. Zoezi hili liendane na kuweka
alama ya pata kila anapobaini kuwa mwanaume/mwanamke anayemchunguza
amepata moja ya vigezo vyake. Lakini pia aweke alama ya kosa kwa kila
kasoro anayoivumilia na ile asiyoivumilia.
TANO - Ajipe
muda wa kutosha kati ya miezi sita na mwaka kumchunguza huyo mwanaume,
kisha aketi chini na aanze kujumlisha alama za vigezo alivyovijiwekea na
jinsi mwanaume huyo alivyopata au kukosa.
Ikibainika
mwanaume aliyechaguliwa amepata zaidi ya nusu ya alama ya vigezo
vilivyowekwa, basi ujue kuwa anafaa. Kuhusu alama chache alizikosa
anaweza kusaidia kuzikamilisha polepole wakati wa maisha ya ndoa.
Lakini
angalizo kubwa kabisa ni kwamba mwanaume/mwanamke akionekana kuanguka
katika kasoro zisizoweza kuvumilia kwa zaidi ya alama tatu. Yaani kwa
mfano ni mlevi, mwizi, muongo, mbishi na katika hizo kashindwa 3, huyu
hafai, ni vema akawekwa kando kwani huwezi kubeba kero 3 kwa pamoja
katika maisha.
SITA - Kusajili mapenzi
yenye malengo yanayotekelezeka. Lazima baada ya kuchunguzana kwa kina
wapenzi watengeneze muongozo wa mapenzi yao. Wasiwe kama wanyama, lazima
mipango ya wapi wametoka walipo na wanapokwenda.
Hata
hivyo watalaam wanasema lazima wapenzi wapime umakini wao kwa vitendo.
Kama wamekubaliana kuoana, suala la mume kwenda kujitambulisha kwa wakwe
na hatua ya kuiendea ndoa ionekane. Usiri usiwepo tena. Kila mmoja
amuone mwenzake kama sehemu ya maisha yake na mara zote wasaidiane kwa
ukaribu.
SABA - Ni vema ndugu
wakashirikishwa ili kuwapa nafasi na wao ya kuamua kama mapenzi hayo ni
budi yakaendelea au yakasitishwa. Ni ukweli ulio wazi kwamba licha ya
wengi kupuuza maamuzi ya ndugu kwa madai ya kuwa hawana nafasi kwa
wapenda nao, lakini uchunguzi unaonesha kuwa wapenzi wengi huacha
kutokana na sumu za ndugu hasa pale wanapokuwa wameonesha kutounga mkono
uhusiano wa wanaotaka kuoana
NANE - Hatua
hii ni ya kuweza kuzungumzia ufanyaji mapenzi, hapa nina maana kama
wapenzi wamejizuia kwa muda mrefu na wanahisi kuchoka wanaweza
kujadiliana kuhusu hilo na kuamua ufanyaji huo wa mapenzi una lengo
gani, kama ni kuburudisha miili basi suala la afya na uzazi salama
litazamwe.
TISA - Kutimizwa kwa ahadi
ya kuoana ni hatua ya tisa ambayo nayo si busara ikachukua muda mwingi
kutekelezeka, kwani ucheleweshaji mwingi wa ndoa nao huvunja moyo na
mara nyingine umewafanya wengi kutoaminiana.
KUMI - Kuamua
kuwa mwili mmoja kwa kuvumilia na kuwa tayari kukabiliana na changamoto
zote za maisha ukiwemo mkwamo na dhiki ambazo huchangia sana ndoa
nyingi kuvunjika. Hapa pia ni wajibu wa wanandoa kuchukuliana udhaifu na
kusaidia, kuwa tayari kujifunza na kujali zaidi upendo kuliko hisia za
mwili ambazo wakati mwingine hudanganya na hivyo kumfanya mwanandoa
asivutiwe na mwenzake.
Mwisho ni kwamba kanuni hizi
huwafaa watu wazima mapenzi ya kitoto hayawezi kujenga misingi hii imara
mara nyingi ni kudanganyana, kuharibiana maisha, kupeana mimba na
maradhi